Kwa mujibu wa ripoti ya kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf, katika khutba za Swala ya Ijumaa alizotoa katika Husseiniya A’dham Fatimiya mjini Najaf Ashraf, akielezea mwezi mtukufu wa Ramadhani alisema: katika mwezi huu tunapaswa kuongeza mwelekeo wetu kwa Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mtume Mtukufu (rehema na amani zimshukie yeye na familia yake):
“Huu ni mwezi ambao mmealikwa katika karamu ya Mwenyezi Mungu na mmewekwa miongoni mwa watu wa heshima ya Mwenyezi Mungu; pumzi zenu humo ni tasbihi, usingizi wenu ni ibada, matendo yenu yanakubaliwa na dua zenu zinajibiwa.”
Alisisitiza kuwa; mwezi huu unapaswa kutumiwa kwa kujijenga upya kiroho na kurekebisha maadili. Mtume Mtukufu alisema:
“Yeyote atakayeboresha tabia yake katika mwezi huu atapata ruhusa ya kupita katika Sirat siku ambayo miguu itateleza.”
Imamu wa Ijumaa wa Najaf Ashraf alivitaka pia vyombo vya habari vya Iraq kuhifadhi heshima ya mwezi wa Ramadhani akisema, kuna mipango ya kuwapotosha vijana kutoka katika maadili ya mwezi huu. Alitaja miongoni mwa hayo utayarishaji wa tamthilia iitwayo “Hamdiya” na mwandishi wa Kibathi aliyekimbia, akiongeza kuwa; tamthilia hiyo ni potofu na yenye ufisadi, na kwamba baadhi ya wabunge wameomba isirushwe hewani. Aliviomba vyombo vya habari vya Iraq kuzuia kuoneshwa kwake na kuwachukulia hatua waliohusika katika kuitangaza.
Kuhusu kile kinachoitwa “Siku ya Mapenzi” (Valentine), alisema kuwa ni njama ya Kimagharibi ya kuwapotosha vijana na kwamba kimsingi ni kumbukumbu ya kasisi aliyepotoka ambaye aliuawa kutokana na kosa la kimaadili. Aliwataka vijana na vyombo vya habari kuepuka kueneza tukio hilo.
Katika sehemu nyingine ya khutba yake, alizungumzia habari ya kuharibiwa kwa kaburi la mwombolezaji wa Imam Hussein, “Hamza Saghir”, akisema tukio hilo halipaswi kuchukuliwa kuwa la mtu binafsi tu, hata kama bado haijajulikana aliyelifanya. Alikumbusha kuwa; waombolezaji na wahubiri ni sauti ya madhehebu na njia ya kuvutia vijana na kuimarisha uhusiano wao na dini na Mwenyezi Mungu. Mtume Mtukufu amesema:
“Kwa hakika kuuawa kwa Hussein kuna joto katika nyoyo za Waumini lisilopoa kamwe.”
Na Imam Ja‘far al-Sadiq alisema:
“Yeyote atakayeimba shairi moja kuhusu sisi, Pepo itamlazimu.”
Katika sehemu nyingine ya khutba, alizungumzia masuala ya kikanda na kumbukumbu ya miaka 47 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, akisema tukio hilo linathibitisha mambo matatu muhimu: umoja wa watu wa Iran, uaminifu wao kwa uongozi, na utayari wao wa kukabiliana na maadui.
Katika khutba ya kidini pia alizungumzia mada ya ukuaji wa kibinadamu kwa msingi wa “muwasaat” (kuhurumiana na kusaidiana), akirejea dua mashuhuri ya mwezi wa Shaaban:
“Na uniruzuku kunisitiri na kumsaidia aliyepungukiwa na riziki Yako kwa kile ulichonipanulia katika fadhila Zako.”
Miongoni mwa hadithi za Mtume Mtukufu inasema:
“Hakamiliki imani ya mmoja wenu mpaka ampendelee ndugu yake kile anachojipendea.”
Na Amirul-Muuminin Imam Ali alisema:
“Hasha tamaa yangu kunishinda na kuniongoza kuchagua vyakula bora, hali ya kuwa katika Hijaz au Yamama kuna watu wasiopata hata kipande cha mkate wala hawajui kushiba.”
Aliongeza kuwa; mtazamo wa dini unaeleza kwamba kutoa na kusaidiana kunasababisha kuongezeka kwa riziki, kama Mwenyezi Mungu anavyosema:
“Ni nani atakayemkopesha Mwenyezi Mungu mkopo mwema ili amzidishie mara nyingi?”
Hili likiwa kinyume na nadharia za kiuchumi za kimada.
Mwisho, alikumbusha kumbukumbu ya kuuawa kishahidi kwa Ayatullah Sayyid Muhammad Muhammad-Sadiq al-Sadr tarehe 19 Februari 1999, akisema kuwa; kuuliwa kwa wanazuoni na maraji' na chama cha Baath ni dalili ya wazi ya tabia ya kupinga Uislamu ya chama hicho, kilichoanzishwa na Michel Aflaq, na kwamba lengo lake lilikuwa kupotosha umma wa Kiislamu kutoka katika njia ya dini na maadili.
Maoni yako